HABARI KIMATAIFA : Mtuhumiwa azua kihoja mahakamani Rwanda
Rwanda imekuwa ikiendedesha harakati za upatanishi na pia
kuwakumbuka waliokufa katika mauaji hayo
Mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Emmanuel
Mbarushimana amekataa uendeshwaji wa kesi yake na mahakama ya Kigali kwa kutoa
pingamizi kwamba hana haki zilizo sawa na mwendesha mashitaka.
Mshukiwa huyo alikabidhiwa Rwanda na nchi ya Denmark mapema
mwezi wa saba mwaka huu ili kujibu mashitaka ya kuhusika katika mauaji ya
kimbari ya mwaka 1994.
Mushukiwa huyo Bwana Emmanuel Mbarushimana amesema kesi yake
haiwezi kusikizwa hadi pale atakapopata haki zilizo sawa na mwendesha
mashitaka.
Hoja yake ilikuwa kwamba ni lazima na yeye aruhusiwe kukaa
badala ya kusimama wakati kesi yake ikisikilizwa na wakati huo huo mwendesha
mashitaka asimame badala ya kukaa kama ilivyozoeleka.
Aidha, amesema kuwa hajafurahia utaratibu unaotumiwa wa
kuingia katika chumba cha mahakama ambapo mwendesha mashitaka na majaji
wanaingia kwa kutumia mlango mmoja kinyume na mushitakiwa.
Mwendesha mashitaka amemshitaki kwa kushiriki katika mauaji
dhidi ya watutsi yaliyotokea katika maeneo mbali mbali katika mkoa wa zamani wa
Butare kusini mwa Rwanda.
Mushukiwa pia ameleta hoja nyingine ya kwamba hana wakili.
Swala hilo la kuwa na wakili lilikuwa limeshajadiliwa katika
kikao cha kesi kilichotangulia ambapo alipewa muda wa kuchagua wakili
anayetaka.
Wakati huo alipewa orodha ya mawakili 500 miongoni mwa
mawakili wanaohudumu hapa nchini na kuikataa.
Alipendekeza kupewa orordha nzima ya mawakili wote kwa
ujumla ili amchague mmoja anayetaka.Kipindi alichokuwa amepewa kuchagua wakili
huyo kilikuwa kimemalizika.
Mahakama imesema kuwa hoja hizo haziwezi kuzuiya kesi hasa
ikiwa ni kesi ya kukiri ama kukana mashtaka dhidi yake;jambo alilokataa kata
kata akisema mahakama haina uhuru wala haki.
Imetangazwa kuwa Uamuzi kuhusu mabishano hayo utatolewa
kesho.
Emanuel Mbarushimana mwenye umri wa miaka 50 alikabidhiwa
Rwanda na mahakama ya Denmark mapema mwezi uliopita ili kujibu tuhuma za
kuhusika kwake katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.::Chanzo Cha habari hii BBC SWAHILIHABARI / NA AGAPE MSUMARI
No comments:
Post a Comment